11 Machi 2021 - 08:45
Wasiwasi wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na kufukuzwa nchini India wakimbizi wa Kirohingya

Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi mkubwa ulionao kuhusiana na mpango wa serikali ya India wa kuwafukuza wakimbizi wa Kirohingya wa Myanmar kutoka katika maeneo ya Jammu na Kashmir.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa sambamba na kueleza wasiwasi wa umoja huo kwa uamuzi wa serikali ya New Delhi wa kutaka kuwafukuza nchini humo wakimbizi 168 umeeleza kwamba, haipasi kuwarejesha wakimbizi mahala ambapo wanafuatiliwa na kusakwa.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, kwa mujibu wa sheria za kimataifa haipaswi kumrejesha mtu katika nchi ambayo kuna hatari ya kupata maudhi, mateso na miamala isiyo ya kibinadamu.

Radiamali hiyo ya Umoja wa Mataifa inafuatia mpango wa serikali ya India wa kutaka kuwarejesha nchini Myamar wakimbizi 168 ambapo imesema itafanya hivyo endapo itathibitika kwamba, wanaishi kinyume cha sheria nchini humo. 

Taarifa ya serikali ya India imesema kuwa, mpango wa kuwarejesha wakimbizi hao ambao ni Waislamu wa jamii ya Rohingya na ambao tayari wametiwa mbaroni unatarajiwa kuanza kutekelezwa siku chache zijazo.

Itakumbukwa kuwa, wimbi jipya la mauaji, mashambulizi na ubakaji wa jeshi la Myanmar katika mkoa wa Rakhine kuwalenga Waislamu wa Rohingya, lilianza tarehe 25 Agosti mwaka 2017 ambapo zaidi ya Waislamu elfu sita waliuawa na wengine elfu nane kujeruhiwa. Aidha zaidi ya Waislamu wengine milioni moja wa jamii hiyo walilazimika kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh.

342/